Monday, January 21, 2013

Wakenya wakana kuhusika katika uporaji NMB Mwanga

Kwa ufupi
Mshtakiwa Kimani, naye alijitetea kuwa siku tukio la uporaji NMB Mwanga likitokea, yeye hakuwepo Tanzania na aliingia nchini Julai 19, 2007 akiwa kama mhamiaji haramu anayelekea Afrika Kusini.


WATUHUMIWA wawili ambao  ni raia wa Kenya na mmoja wa Tanzania, wanaodaiwa kupambana na polisi kwa saa sita katika nyumba moja jijini Arusha mwaka 2007, wamekanusha kuwepo katika nyumba hiyo siku ya tukio.

Upande wa mashtaka, unawatuhumu raia hao wa Kenya na Watanzania watano , kushiriki katika tukio la uporaji wa Sh239 milioni katika Benki ya NMB Mwanga, uporaji ulioambatana na mauaji.

Mashahidi wa upande wa mashtaka walikuwa wakiwatuhumu raia hao wa Kenya, Samwel Saitoti na Peter Kimani na Mtanzania Elizabeth Msanze, kupambana nao kwa silaha nzito Julai 20 mwaka 2007.
Katika ushahidi wao, mashahidi hao wanadai kuwakuta watuhumiwa wakiwa na  mabomu mawili ya kutupwa kwa mkono, bunduki mbili aina ya SMG, risasi 85 na fulana zinazozuia risasi kupenya mwilini.

Hata hivyo, wakati wakijitetea kwa wiki zima iliyomalizika Ijumaa iliyopita, washtakiwa hao wamekanusha vikali kuwapo katika nyumba hiyo na kusisitiza kuwa ushahidi dhidi yao ulikuwa ni wa kutunga.

Mshtakiwa wa kwanza, Saitoti alijitetea kuwa hata siku uporaji huo ulipotokea Julai 11 mwaka 2007, yeye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta (KNH) nchini Kenya na hakuwapo nchini.

Alijitetea kuwa alikuja nchini Julai 19 kufuatilia deni lake la Sh800,000 kutoka kwa mzee Ladislaus na kukamatwa siku hiyo hiyo saa 7:00 mchana jijini Arusha. Alisema baadaye aliwekwa mahabusu hadi alipofikishwa kortini.

Mshtakiwa Kimani, naye alijitetea kuwa siku tukio la uporaji NMB Mwanga likitokea, yeye hakuwepo Tanzania na aliingia nchini Julai 19, 2007 akiwa kama mhamiaji haramu anayelekea Afrika Kusini.

Alisema Dola 8,145 za Marekani alizokamatwa nazo ni mali yake na kuiomba mahakama imwachie huru na kuamuru arejeshewe fedha hizo kwani hata katika uporaji huo, hakuna Dola zilizoibwa.

Mshtakiwa wa tatu, Calist Temu ambaye anatuhumiwa kuwa aliwakaribisha nyumbani kwake watuhumiwa walipora fedha hizo na mgawo wa fedha hizo kufanyikia nyumbani kwake, alikanusha tuhuma hizo.

Temu ambaye ni mfanyabiashara mashuhuri wa Sanya Juu wilayani Siha, alidai Julai 12,2007 ambayo inadaiwa watuhumiwa waligawana fedha nyumbani kwake, hakukuwa na mgeni aliyefika siku hiyo.

Mshtakiwa Elizabeth maarufu kama Bella ambaye inadaiwa alikamatwa katika nyumba ya Njiro baada ya mapambano makali na polisi, naye alikanusha vikali kulala katika nyumba hiyo siku hiyo. Washtakiwa Elizabeth Msanze, Julliana Msanze na Ntibasalile Msanze walikanusha kuwahifadhi raia hao wa Kenya na watuhumiwa wengine wakidai huo ulikuwa ni ushahidi wa uongo na wa kutunga.

Mshtakiwa Julliana alienda mbali zaidi alipomtuhumu shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka, Linus Sinzumwa kuwa alimuunganisha kwenye kesi baada ya kumnyima rushwa ya Sh10 milioni.

Baada ya washtakiwa kumaliza kujitetea, mahakama iliwaagiza mawakili wa Serikali, Prosper Rwegerera na Tamari Mndeme wanaoendesha kesi hiyo majumuisho ya kesi hiyo Februari 28 mwaka huu.

Mahakama hiyo inayoongozwa na jopo la mahakamu watatu, Pantrine Kente, Aziza Temu na John Nkwabi umewataka washtakiwa kujibu hoja za mawakili hao kabla au Machi 15 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment