Tuesday, May 28, 2013

Treni yaua mchumi Dar es Salaam

Gari aina ya CRV Honda yenye namba za usajili T 680 ARK likiwa kwenye kituo cha Polisi cha Tazara, Dar es Salaam baada ya kugonga treni eneo la Moshi Bar na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wawili kujeruhiwa, jijini jana. (Picha na Fadhili Akida).
Gari aina ya CRV Honda yenye namba za usajili T 680 ARK likiwa kwenye kituo cha Polisi cha Tazara, Dar es Salaam baada ya kugonga treni eneo la Moshi Bar





MCHUMI wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Elias Kitundu (39) amekufa papo hapo huku mkewe Agness Msoka (37) na mtoto wao Samson Kitundu (17) wakijeruhiwa, baada ya gari lao kugonga ‘treni ya Mwakyembe’ jana alfajiri eneo la Moshi Baa Ilala, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo lililotokea saa 11.46 na kuthibitishwa na Kamanda wa Kikosi cha Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA), Rashid Seif, chanzo chake ni uzembe wa dereva wa gari aliyekatisha reli wakati treni ikiwa karibu.

Ilielezwa kuwa lengo la dereva huyo ambaye ni mke wa marehemu, alikuwa akiendesha kwa kasi gari hilo namba T 680 ARK aina ya Honda, akiwahi kuvuka upande wa pili wa reli, ili kumwahisha mtoto wao anayesoma Sekondari ya Airwing, ndipo ilipogonga treni na kusababisha mauti ya mchumi huyo.

“Ilionekana dereva hakutaka ushauri wa mtu yeyote, kwani licha ya watu kumpigia kelele na madereva wa magari mengine kumwashia taa wakimtaka asimame, hakutaka kusikiliza ushauri huo,” alisema mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Salum Makiya.

Mmoja wa wahudumu wa treni hiyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa yeye si msemaji, alisema akiwa ndani ya treni akitoa huduma, alisikia kishindo na mkwaruzo na alipochungulia dirishani aliona gari likikokotwa na treni umbali wa takribani meta 50 kabla ya kusimama.

Kamanda Seif, aliitaja namba ya treni iliyohusika katika ajali hiyo kuwa ni 5111 yenye injini namba BHF- 002, na ilikuwa ikiendeshwa na David Ngonyani akisaidiwa na Moshi Hilary ikitoka Kipunguni kwenda Jet Lumo.

Alisema ajali hiyo ilisababishwa na uzembe na kuthibitisha kifo cha mchumi huyo kilichotokea papo hapo na mkewe na mtoto kujeruhiwa na baada ya muda mfupi wote walikimbizwa katika Hospitali ya Amana.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana baadaye Amana, mtoto huyo aliruhusiwa baada ya kupata matibabu ya michubuko huku mama yake akihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na majeraha aliyopata yakiwamo ya kuvunjika miguu.

By Oscar Job

No comments:

Post a Comment