Saturday, January 19, 2013

Mawaziri waibua madudu ya kutisha bandarini Dar

Kwa ufupi

Kutokana na kubadilishwa kwa kipengele hicho, TPA italazimika kutoa kiasi cha Dola 3 milioni ambazo ni sawa na takriban Sh4.8 bilioni katika kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kukarabati mtambo huo.

Kaimu MKurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Madeni Kipande (Kulia) akitoa maelezo kwa Mawaziri waliotembelea uongozi wa TPA ili kufahamu matatizo na changamoto zake jijini dar es Salaam jana, kutoka kushoto ni Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa , Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison  Mwakyembe na  Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda 
MAWAZIRI wanne wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wameipa siku mbili Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari (TPA) kueleza sababu za kubadilishwa kwa kipengele cha mkataba wa ujenzi wa Mtambo wa Kupakua Mafuta katika Meli (SPM) bandarini.

Kutokana na kubadilishwa kwa kipengele hicho, TPA italazimika kutoa kiasi cha Dola 3 milioni ambazo ni sawa na takriban Sh4.8 bilioni katika kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kukarabati mtambo huo.

Pia wameagiza moja ya mashine inayotumika kukagua mizigo inayoingia katika bandari hiyo, iliyopelekwa katika Bandari ya Tanga miaka miwili iliyopita irejeshwe mara moja, kwa kuwa haifanyi kazi yoyote na kwamba, kukosekana kwake katika Bandari ya Dar es Salaam kunasababisha msongamano wa mizigo.

Maagizo hayo yalitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene baada ya kufanya ziara fupi ya pamoja jana katika Bandari ya Dar es Salaam.

Wakati mawaziri hao wakitoa maagizo hayo, TPA ilieleza kuwa ili kuboresha huduma za bandari zote zilizopo nchini, inahitaji kupatiwa mkopo wa Dola 4 bilioni za Marekani.

Sakata la kunyofolewa kwa kipengele hicho cha mkataba, liliibuka baada ya Dk Mwakyembe kumbana Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Madeni Kipande akieleza kwamba, licha ya mamlaka hiyo kukabidhiwa mtambo huo na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Leighton ya Singapore, inaonekana kuna kipengele ndani ya mkataba huo kimeondolewa.

“Awali mkataba ulieleza wazi kwamba baada ya kampuni hii kukamilisha kazi yake ya kuweka mtambo ingetuachia vifaa vya ukarabati wa mtambo ambavyo vina thamani ya Dola 300 milioni, lakini kampuni hii haikuacha, kwa nini” alihoji Dk Mwakyembe na kuongeza:

“Vifaa hivi vya ukarabati tungevitumia kwa muda wa miaka miwili, sasa tunataka kujua aliyekichomoa kipengele hiki ni nani, ili na sisi tumchomoe.”

Baada ya kauli hiyo ya Dk Mwakyembe, Simbachawene alizidi kumbana Kaimu Mkurugenzi huyo akisema: “Na kwa nini mkataba ubadilishwe wakati hicho kipengele ndiyo kilikuwa moja ya sababu za mwekezaji kupata hiyo zabuni ya ujenzi wa mtambo, hapa TPA si kuna wanasheria, iweje litokee hili?”

Akijibu swali hilo, Kipande alisema kuwa baada ya zabuni hiyo kupita kipengele hicho kiliondolewa, hivyo kuilazimu TPA kuingia gharama za kufanya matengenezo.

“Nilichokieleza ndiyo hicho… Ila naomba muda ili niliandike kwa maandishi suala hili,” alisema Kipande.

Licha ya maelezo hayo, Dk Mgimwa alimwambia Kipande kuwa wao wanahitaji taarifa sahihi ili wajue aliyekiondoa kipengele hicho kwa kuwa hali hiyo inaonyesha wazi kwamba bandari inahujumiwa, huku akiitika Bodi ya TPA kueleza hatua ilizochukua hadi sasa.

Baada ya mvutano wa takriban dakika 10, Dk Mwakyembe aliitaka Bodi na Menejimenti ya TPA kukutana kwa dharura na Jumatatu asubuhi iwe imepata jibu na kumpelekea ofisini kwake kwa maandishi.

“Hii ni hujuma kwa taifa na wananchi kwa jumla. Tunataka kumjua huyo mtu aliyehusika kuchomoa kipengele hiki, Jumatatu asubuhi nataka taarifa za aliyehusika, ziwe mezani kwangu,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:

“Taarifa hiyo nitaipeleka kwa mawaziri wote nilioambatana nao leo, halafu tutatoa kauli ya pamoja ya jinsi ya kufanya, au kuangalia kama kutakuwa na uwekekano wa kulihamishia suala hili Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).”

Dk Mwakyembe pia alisema kwamba kuanzia sasa ni marufuku kwa kampuni za ndani na nje ya nchi kupewa kibali cha kujenga Bandari za Nchi Kavu kwa ajili ya kuhifadhia magari na makontena, eneo lililo karibu na Bandari, kwa maelezo kuwa hazisaidii kuondoa mrundikano wa mizigo bandarini.

“Tunataka maeneo haya yajengwe nje ya mji mfano ni eneo la Kibaha na siyo karibu na bandari,” alisema Dk Mwakyembe.

Ukaguzi wa mizigo

Kwa upande wake Dk Mgimwa aliyeonekana kuwa mkali aliendelea kumbana Kaimu Mkurugenzi wa TPA, safari hii akitaka kujua utaratibu wa ukaguzi wa mizigo katika bandari hiyo.

Akijibu swali hilo, Kipande alisema kazi ya ukaguzi hufanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwamba mashine za ukaguzi zipo mbili, lakini moja imepelekwa mkoani Tanga, ambako hivi sasa haitumiki.

Baada ya kauli hiyo Dk Mgimwa alisema kwamba wanataka kupata taarifa za kutokusanywa ipasavyo kwa mapato katika bandari hiyo.

“Mizigo yote inayoingia na kutoka ni lazima ikaguliwe; Serikali ina nia ya dhati kabisa ya kuwasaidia wananchi. Ni lazima tufanye kikao cha pamoja ili kujua wapi mnapokwama na kuona jinsi ya kuweka mambo sawa,” alisema Dk Mgimwa.

Naye Dk Kigoda alisema kuwa kinachotokea katika bandari hiyo kinatokana na baadhi ya watendaji wake kutokuwa waadilifu, huku akisisitiza kuwa bandari siyo eneo la kufanyia mchezo kwa sababu ni eneo linaloweza kuliingizia taifa fedha nyingi.

“Ili kufanikisha hili na mimi naliagiza Shirika la Viwango Nchini (TBS) kufanya kazi saa 24, pia lipewe eneo katika bandari hii ili kujenga ofisi kwa ajili ya ukaguzi,” alisema Dk Kigoda.

Baada ya maelezo hayo, Dk Mwakyembe aliagiza kuwa mashine hiyo ya ukaguzi wa mizigo irejeshwe Dar es Salaam akisema: “Ndiyo maana nasema kuna hujuma hapa, wapo watu wanaofaidika kwa sababu tu ya mizigo kuchelewa kutoka Bandarini, hiki kifaa kirudishwe haraka hapa na siyo kuwarushia mpira watu wa TRA.”

Maelezo ya TPA

Awali wakati akielezea changamoto na mikakati ya TPA, Kipande alisema kuwa ili kuboresha Bandari ya Tanga, Dar es Slaam, Mtwara pamoja na bandari zilizopo Ziwa Tanganyika, Victoria na Nyasa, mamlaka hiyo inahitaji mkopo wa Dola 3 hadi 4 bilioni.

“Tukipewa fursa ya kupata fedha hizi baada ya miaka sita tutapiga hatua kubwa, pia mkopo huu uwe na riba nafuu ambayo itatufanya tulipe taratibu kwa miaka takriban 30,” alisema Kipande.

Changamoto

Akielezea changamoto walizonazoikabili TPA alisema kuwa Bandari ya Dar es Salaam ina kina kifupi cha maji na kujaa mchanga, hivyo meli kubwa za kimataifa zinashindwa kufika jambo ambalo linaikosesha nchi mapato.

Alitolea mfano kuwa Bandari ya Dar es Salaam ina sehemu 12 za kuegeshea meli, lakini zinazoweza kuegeshwa kwa wakati mmoja ni nne kutokana na maeneo mengine kuwa na kina kifupi cha maji.

“Eneo la Mjimwema pale Kigamboni lina kina kirefu cha mita 17 na eneo kubwa la ujenzi wa matangi ya mafuta, hivyo kama bandari ikipanuliwa itakuwa na uwezo wa kupokea meli nyingi zaidi zenye uwezo wa kubeba kontena 10,000,” alisema Kipande.

Alisema kuwa Bandari za Tanga na Mtwara nazo zina tatizo kama la Dar es Salaam, huku akipendekeza nazo zifanyiwe ukarabati na kupanuliwa.

“Tukiwa na reli tunaweza kusafirisha mizigo kwenda mikoani ili nchi zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kama Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda, wachukue mizigo yao katika mikoa hiyo, utaratibu huo utawaondolea gharama,” alisema Kipande.

Alisema mikakati waliyonayo hivi sasa ni TPA kuwa na treni itakayowekwa kwa ajili ya kusafirisha mizigo katika maeneo maalumu watakayoyatenga kwa ajili ya kuhifadhia mizigo hiyo, kupanua bandari na kujenga maeneo ya kuhifadhia mizigo mkoani Tabora na Singida.

No comments:

Post a Comment