Wednesday, January 16, 2013

KKKT yamkataa kigogo wa Jimbo


    By John Mhala, Arusha

HALMASHAURI Kuu ya Usharika wa Ngateu katika Jimbo la Arusha Magharibi Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), imemkataa mmoja wa vigogo wa Jimbo hilo (jina linahifadhiwa).

Uamuzi wa kumkataa kigogo huyo ambaye ni Mchungaji ulitangazwa Jumapili jioni baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Usharika huo kilichofanyika kwa saa tisa kanisani hapo.

Mchungaji huyo alikataliwa na huduma zake za kiroho katika Usharika huo kwa madai kuwa ndiye chanzo na mchochezi wa mgogoro unaoendelea ndani ya Kanisa hilo.

“Kuanzia leo (Jumapili) tunatangaza rasmi kwamba hatumtaki Mchungaji (anatajwa) pamoja na huduma zake zote kwa kuwa tumebaini kuwa yeye ndiye chanzo na mchochezi wa mgogoro huu kwa manufaa yake binafsi,” ilieleza sehemu ya taarifa ya kikao cha Halmashauri hiyo.

Mmoja wa wajumbe aliyehudhuria kikao hicho ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema walibaini kuwa Mchungaji huyo anahusika moja kwa moja na mgogoro unaoendelea na hawataki kumwona katika jimbo hilo.

Maazimio mengine ya kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 120 kutoka mitaa mbalimbali ya Usharika huo ni pamoja na kufanya maandamano, ikiwa uongozi wa Dayosisi utashindwa kumrejesha kazini Mchungaji Philemon Mollel aliyekuwa Mchungaji Kiongozi katika Usharika huo.

Mchungaji Mollel alisimamishwa kazi na kuzuiwa kufanya kazi za kichungaji katika Kanisa hilo kuanzia Desemba 24, kwa kilichoelezwa kuwa ni makosa yasiyovumilika ndani ya Kanisa.

Kabla ya kusimamishwa kazi Mchungaji huyo, kuliibuka mgogoro katika Kanisa hilo baada ya moja ya benki za biashara (jina tunalo) kuipa Dayosisi hiyo muda hadi Desemba 31 mwaka jana, iwe imelipa deni la Sh bilioni 11, vinginevyo mali zake zingepigwa mnada.

Kutokana na taarifa hiyo ya benki, Kanisa lilitoa waraka wa Askofu ambapo waumini zaidi ya 600,000 walitakiwa kila mmoja achangie Sh 20,000 ili kunusuru mali za Kanisa zilizo hatarini kufilisiwa, baada ya Hoteli ya Corridor Springs, mali ya Kanisa hilo kudaiwa fedha hizo.

Baada ya waraka huo, baadhi ya waumini akiwamo Mollel wakitaka waliohusika na uzembe uliosababisha deni hilo wawajibike kabla ya waumini kutoa mchango huo.

Kutokana na msimamo huo, Mollel alitakiwa kuomba radhi na alipokataa, alisimamishwa kazi na kuvuliwa madaraka ya kuhudumia Usharika wa Ngateu aliokuwa akihudumia.

“Tumewapa viongozi wetu wa Dayosisi hadi Januari 20, wawe wamemrudisha kazini Mchungaji Mollel bila masharti na Katibu Mkuu wa Dayosisi Israel ole Karyongi asimamishwe kazi kupisha uchunguzi huru, la sivyo tutafanya maandamano.

“Tutafanya maandamano baada ya kushauriana na wanasheria wetu na hakuna anayeweza kutuzuia hata kama polisi watazuia, kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hiyo ni haki yetu,” alisisitiza mjumbe ambaye naye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Alisema masharti mengine waliyotoa ndani ya siku hizo ni kutaka Bodi ya Arusha Corridor Springs inayoongozwa na Karyongi ivunjwe ili kupisha uchunguzi huru na watakaobainika kuhusika na hujuma za mali za Dayosisi wachukuliwe hatua za kisheria.

Gazeti hili halikumpata Mchungaji huyo kuelezea tuhuma hizo baada ya simu ya mkononi kuzimwa kwa kuwa katika kikao cha Wachungaji wa Dayosisi. Gazeti hili litaendelea kumtafuta kupata maelezo zaidi kuhusu msimamo huo wa Usharika wa Ngateu.

No comments:

Post a Comment