Sunday, February 10, 2013

MAGUFULI AFAGILIWA MBELE YA RAIS

 Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.KATIBU Muhtasi wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Singida, Sarah Mkumbo amemfagilia Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli mbele ya Rais Jakaya Kikwete, akisema ni mchapa kazi na kazi zake zinaonekana nchi nzima.

Mkumbo mwenye ulemavu wa viungo, pia amempongeza na kumshukuru Rais Kikwete na kumwambia Mungu ndiye aliyemchagua, kutokana na kujali watu wa aina mbalimbali. Alisema hayo jana wakati akikabidhiwa pikipiki ya magurudumu matatu iliyotolewa na Rais Kikwete, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa takribani miezi miwili iliyopita, baada ya kufanya ziara mkoani Singida na kumwona mtumishi huyo wa Tanraods.

“Ni Mungu aliyekuteua. Nina hakika wewe nikiongozi shujaa unayejali kila mtu. Mungu akupe afya njema uendelee kuona na wengine,” alisema. Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Waziri Magufuli, mtumishi huyo wa Tanroads alisema, “hongera kumteua Waziri Magufuli.

Kazi zake zinaonekana umechagua mchapakazi.” Mtumishi huyo ambaye amefanya kazi Tanroads kwa zaidi ya miaka 30, aliomba Serikali iangalie wenye ulemavu na kuwawezesha kupata mahitaji yao. Alisema pikipiki hiyo itamwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema amepata pia faraja kwa kuwa ana uhakika chombo hicho cha usafiri, kitamwezesha kufika ofisini kwa urahisi. Wakati huo huo, Rais Kikwete jana ‘aliteta’ na baadhi ya wabunge wa mkoa wa Mtwara katika Ikulu ndogo ya mjini Dodoma.

Hata hivyo, hapakuwepo taarifa rasmi juu ya lengo la kikao hicho. Awali, waandishi waliofika Ikulu kwa ajili ya kuhudhuria hafla ya kukabidhi pikipiki ya magurudumu matatu kwa Katibu Muhtasi huyo wa Tanroads, waliambiwa Rais alikuwa na kikao na wageni wengine.

Baada ya kikao hicho kumalizika, walionekana wadau hao wa Mtwara wakitoka kwenye lango la Ikulu ndogo. Miongoni mwa wabunge ambao mwandishi alishuhudia wakitoka Ikulu baada ya kikao na Rais ni Anna Abdallah (Viti Maalumu), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) na Agnes Hokororo (Viti Maalumu). Hivi karibuni ziliibuka vurugu mkoani Mtwara zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu mbalimbali wakiwemo wabunge.






No comments:

Post a Comment