Prof.Sospeter Muhongo |
DODOMA, TANZANIA
Wizara ya Nishati na Madini imetenga jumla ya sh. bilioni 8.9 kwa
dhamira ya kuwainua wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kukuza kipato
chao na hivyo kuboresha maisha yao. Aidha, jitihada za kuwainua
wachimbaji wadogo zinalenga pia kuinua pato la taifa kutokana na
kuongezeka kiwango cha kodi na tozo mbalimbali zinazopaswa kulipwa na
wachimbaji hao kwa serikali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
alipokuwa akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano mkuu wa mwaka wa
wachimbaji wadogo wa madini nchini, uliofanyika mjini Dodoma tarehe sita
na saba mwezi huu.
“Tunayo dhamira ya dhati kuwasaidia ili maisha yenu yaboreke na pia ili
kukuza pato la taifa hili”, alisisitiza Waziri Muhongo na kuongeza kuwa
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ndilo limepewa jukumu la kusimamia
mipango ya uendelezaji wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na taasisi
nyingine mbalimbali zinazohusika na sekta ya madini.
Hata hivyo Profesa Muhongo amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini
kuhakikisha wanasajili biashara zao, kuanisha mapato yao, pamoja na
kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazowahusu ili taifa liweze kunufaika
na rasilimali hiyo ya madini. Alisisitiza kuwa wachimbaji watakaofuata
vigezo hivyo ndiyo tu watakaopata misaada ya aina mbalimbali ikiwemo
mafunzo na mikopo kutoka serikalini na wadau wengine wa maendeleo.
Kwa upande wao, wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili, ambao
ni viongozi na wawakilishi wa vyama vya wachimbaji madini kutoka mikoa
yote nchini, waliahidi kuyafanyia kazi maagizo hayo ya Waziri kwa
manufaa yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment