Sunday, January 13, 2013

Mume amuunguza sehemu za siri mke wake



Kwa ufupi
“Siku ya tukio hilo alikoka moto akachukua nondo ya kuweka alama kwenye ng’ombe,  akaniambia ingia ndani mke mwenzako anakuita, nilipoingia ndani naye akaingia na kufunga mlango akaniingiza hiyo nondo ya moto,”

 MWANAMKE mkazi wa Kijiji cha Matui, wilayani Kiteto, mkoani Manyara ameponea chupuchupu kuuawa baada ya mume wake kumchoma na chuma cha moto sehemu za siri kutokana na wivu wa mapenzi.

Mwanamke huyo alifanyiwa kitendo hicho juzi usiku kwenye kijiji hicho, baada ya mume wake  kumtuhumu kuwa ana uhusiano wa mapenzi na msaidizi wao wa nyumbani.
Akizungumza kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kiteto juzi, wakati akipatiwa matibabu mwanamke huyo alisema hivi sasa anasikia maumivu makali.

Alisema alipofanyiwa kitendo hicho alipoteza fahamu kwa muda mrefu, kwani alitokwa na damu nyingi na alizinduka baada ya kufikishwa hospitalini hapo iliyopo umbali wa kilomita 32 kutoka nyumbani kwake.

Aliongeza kuwa kabla ya kufanyiwa kitendo hicho, kila mara mume wake alikuwa anamweleza kuwa amesikia tetesi kuwa ana uhusiano wa mapenzi na msaidizi wa kazi, hivyo atamfanyia kitu ambacho hatakisahau.

“Siku ya tukio hilo alikoka moto akachukua nondo ya kuweka alama kwenye ng’ombe,  akaniambia ingia ndani mke mwenzako anakuita, nilipoingia ndani naye akaingia na kufunga mlango akaniingiza hiyo nondo ya moto,” alisema.

Daktari wa hospitali hiyo, Godfray Mbise alisema mwanamke huyo amepata kilema cha maisha baada ya kufanyiwa kitendo hicho cha kikatili, kwani ameachiwa majeraha sehemu za siri, mapajani na mgongoni.

Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Matui, Kidawa Athuman alisikitishwa na kitendo cha Polisi wa Kituo cha Matui kutochukua jambo hilo kwa uzito.

Athuman alisema askari hao wanashindwa kumchukulia hatua mwanaume aliyefanya kitendo hicho, kutokana na nguvu kubwa ya uchumi aliyonayo.

Pia, alisema kijana huyo msaidizi wa kazi ambaye anahisiwa kuwa alikuwa na uhusiano na mwanamke huyo, naye alichomwa moto sehemu ya taya na alitoroshwa katika maboma ya Kimasai akitibiwe ili kuficha jambo hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa alisema hajapata taarifa za tukio hilo na kwamba, atazifuatilia ikufahamu hatua zilizochukuliwa baada ya kutokea jambo hilo.
“Ndiyo kwanza wewe unanipa habari hizi, ngoja nizifuatilie kisha nitakujulisha kinachoendelea lakini hadi hivi sasa (jana) bado sijapewa taarifa yoyote kuhusiana na kitendo hicho,” alisema KMpwapwa.

No comments:

Post a Comment