By Veronica Mheta, Arusha
Mama Salma Kikwete |
MKE wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka watafiti wa masuala ya afya ya mama na mtoto, madaktari pamoja na wauguzi kuzifanyia kazi changamoto wanazokutana nazo ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
Aidha wakunga na madaktari wameaswa kuwa na lugha nzuri zitakazowezesha wanawake kujifungua kwa usalama badala ya kuwapiga vibao na wengine kuwarudisha nyumbani wakisubiri uchungu ili wajifungue.
Mama Salma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Wanawake na Maendeleo (WAMA), alisema hayo jana jijini hapa wakati alipokuwa akifunga mkutano wa pili kimataifa uliohusu kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Mkutano huo unafanyika jijini Arusha kwa siku tatu kuanzia jana na unahudhuriwa na wajumbe 700 kutoka nchi 68 duniani.
Alisema ni vyema wataalamu wa masuala ya afya wafanyie kazi changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wanawake wakati wa kujifungua, ili kupungua vifo vya mama na mtoto vinavyozuilika ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake kumhudumia mwanamke.
“Serikali kila mwaka inaongeza fedha katika sekta ya afya lakini kama wataalamu mjiulize vifo hivi vinatokana na nini na baada ya mkutano huu kila mmoja wenu aondoke na jibu zuri la kuwasaidia wanawake wasife kutokana na uzazi.
“Tunataka mwanamke aishi na si kufa kwasababu ya kumleta kiumbe duniani, lazima tuokoe maisha ya mama na mtoto,’’ alisisitiza.
Mshauri wa Masuala ya Afya kutoka Hospitali ya CCBRT, Brenda D’mello alisema si busara kwa wauguzi au baadhi ya madaktari kutoa lugha zisizofaa kwa wajawazito au kuwapiga vibao wanawake ili wajifungue. Aliwaasa kuachana na tabia hizo na badala yake watoe huduma bora kwa wanawake.
No comments:
Post a Comment