Sunday, February 3, 2013

Rais Kikwete asema gesi haiendi Bagamoyo

RAIS Jakaya Kikwete 
Kwa ufupi

“Ujenzi wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu. Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatakayotokana na

Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa gesi itakayochimbwa mkoani Mtwara haitapelekwa Bagamoyo kama ambavyo baadhi ya watu walivyokuwa wakidai.


Kikwete alisema hayo katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Januari kwa taifa ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, uliozua mgogoro.


Alisema kuwa kuna watu waliosema kwamba gesi inapelekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali.


“Ujenzi wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu. Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatakayotokana na gesi hiyo. Na wengine wakasema gesi inapelekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba Rais anapeleka gesi kwao,” alisema Kikwete na kuongeza:


“Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo. Pili, ukweli ni kwamba pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kubaki.”
Alifafanua kuwa gesi itakayopelekwa Dar es Salaam ni asilimia 16 ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa miaka ishirini ijayo na kwamba asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.


“Kwa sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa na wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka mingi ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na vile vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha. Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha umeme wa megawati 15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba, Newala, Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote hivi sasa,” alisema Kikwete.


Rais Kikwete aliongeza: “Nayaeleza yote haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa tunawathamini sana na kuwajali. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza na kuwatupa mkono wananchi wa mikoa ya Kusini. Aidha, sitakuwa tayari kuwaruhusu watu au mtu yeyote serikalini kuwapuuza wananchi wa mikoa ya Kusini au mkoa wo wote hapa nchini. Hiyo haitakuwa sawa.”


Alisema kwamba, kutokana na msimamo wake huo ndiyo maana Serikali imeelekeza nguvu na rasilimali zake nyingi katika mikoa iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa na kwamba kazi ya ujenzi wa barabara za lami iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera inajieleza yenyewe.


Alitaja pia mipango ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kufikia hadhi ya kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa kuwa ni ushahidi mwingine.
Katika hotuba hiyo Rais Kikwete alizungumzia safari zake za Ufaransa, Uswisi na Ethiopia akisema kuwa safari hizo zilikuwa na manufaa makubwa kwa taifa.


Alisema kuwa katika safari ya Ufaransa licha ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki, wawekezaji wengi wakubwa wameonyesha nia ya kuja kuwekeza nchini na kwamba wamekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa ushirikiano.


Kuhusu mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika Davos, Uswisi, Rais Kikwete alisema mkutano huo umeihakikishia Tanzania ushirikiano katika kuendeleza juhudi za kuleta mapinduzi ya kijani ili kujihakikishia usalama wa chakula, kupunguza umaskini vijijini na kukuza uchumi wa nchi yetu.


Katika hatua nyingine, Salum Maige kutoka Geita anaripoti kuwa madiwani wa Halmashauri za Wilaya za Geita na Nyang’hwale, mkoani Geita, wameitahadharisha Serikali kuwa iwapo itaruhusu gesi kubaki mkoani Mtwara, wao wataandamana kuzuia dhahabu inayochimbwa Geita na kampuni za kigeni, isitoke mkoani humo.

Gervas Kabulu, Diwani wa Kata ya Katoro ambaye alivuliwa uanachama wa Chadema na Diwani wa Kata ya Nzera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joseph Msukuma walitoa hoja hiyo katika Kikao cha Baraza la Madiwani wa wilaya hizo.


Madiwani hao walitoa hoja hizo juzi katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa wilaya hizo, kilichojadili taarifa za kamati mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mipango yake.
Katika kikao hicho Kabulu alitaka madiwani wawahamasishe wananchi waandamane kupinga dhahabu inayochimbwa na kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) isisafirishwe kwenda nje ya mkoa wa Geita.


“Mheshimiwa mwenyekiti kama Mtwara wameandamana, kwa nini tusiwahamasishe wananchi tuandamane, na sisi tuzuie dhahabu yetu kupelekwa Dar es Salaam?”alisema akihoji Kabulu.

Hata hivyo, katibu wa baraza hilo la madiwani, Ali Kidwaka alisema alitaka suala la gesi liachwe kwa Serikali na kwamba dhahabu ya Geita inawanufaisha wananchi wa Geita na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa madiwani hao, Elisha Lupuga alipinga kauli ya diwani Kabulu ya kutaka kuandamana akisema kuwa anaunga mkono kauli ya Serikali ya gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa kuwa inanufaisha wananchi wote.

Kwa upande wake Msukuma alisema kama Serikali itawakubalia wananchi wa Mtwara kuwa gesi ibaki mkoani humo na wao wako tayari kuwahamasisha wananchi wa Geita kufanya maandamano ya amani kupinga dhahabu kutoka Geita.

Sakata la kusafirisha gesi kupelekwa Dar es Salaam lilizua vurugu kubwa hadi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokwenda kuituliza hali hiyo mkoani Mtwara.

No comments:

Post a Comment