Saturday, January 12, 2013

Wauguzi washikilia msimamo Kenya

Kwa ufupi

Kauli hiyo ilitolewa siku chache baada ya mahakama kuondoa haki yao ya kuandaa mgomo iliyotolewa kwa wauguzi wiki iliyopita ambayo iliagiza wafanyakazi hao kurudi kazini.


WAUGUZI katika hospitali za umma nchini Kenya wamekaidi amri ya mahakama iliyowataka warudi kazini na kuapa kuwa wataendelea na mgomo wao.

Kauli hiyo ilitolewa siku chache baada ya mahakama kuondoa haki yao ya kuandaa mgomo iliyotolewa kwa wauguzi wiki iliyopita ambayo iliagiza wafanyakazi hao kurudi kazini.

Licha ya kuwa mahakama ilitoa amri, wauguzi hao waliopo Mkoa wa Pwani walisisitiza kwamba hawatarudi kazini hadi wapate maagizo kutoka kwa maofisa wa kitaifa wa chama chao kuhusu amri ya mahakama.

Kwa upande wa ofisa wa Tawi la Pwani, Peter Moroko alisema kuwa watasubiri hadi Katibu Mkuu wa chama kisichosajiliwa cha Kenya National Union of Nurses (KNUN) Seth Panyako, atoe agizo la kurudi kazini.

Wiki mbili zilizopita, mahakama iliagiza Serikali ishauriane na wauguzi kwa lengo la kutatua shida zao lakini Serikali ikarudi mahakamani na kutoa agizo kwa wauguzi hao warudi kazini.

Wauguzi hao waliendelea kusimama kidete kudai haki zao, huku wagonjwa katika hospitali za umma wakiendelea kuteseka bila kuhudumiwa.

Wagonjwa wengi walilazimika kutafuta matibabu katika hospitali binafsi na kukubali kutozwa fedha nyingi.

Kutokana na hospitali za binafsi kupandisha gharama za huduma ilisababisha baadhi ya wagonjwa kushindwa kulipa bili. Mmoja wa wagonjwa, Sarah Njeri alizuiliwa katika Hospitali ya Axis Nursing Home, iliyopo Mwembe Tayari mjini Mombasa baada ya kushindwa kulipa bili ya Sh40,000 baada ya kujifungua.

Njeri alisema kwamba mtoto wake alifariki baada ya wauguzi kukataa kumhudumia katika Hospitali ya Mkoa ya Pwani alikolazwa kabla ya kuhamishiwa ya kibinafsi.

Nyahururu huduma katika hospitali ya wilaya zilisitishwa na wauguziwaligoma kufanya kazi isipokuwa wauguzi wakuu pekee ndio walikonekana wakitoa huduma .

No comments:

Post a Comment