
KUMEKUWEPO na sintofahamu nyingi sana kuhusu suala la gesi ya Mtwara inayotarajiwa kuchimbwa katika mkoa huo na kusafirishwa moja kwa moja kuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi.
Imeelezwa kuwa nia ya Serikali kupendekeza kusafirishwa kwa gesi kwa njia ya bomba kutoka mkoani Mtwara hadi jijini Dar es Salaam ni kwa sababu jiji hili la Dar lina mitambo mingi ya kufua umeme na pia jiji hilo linachangia karibu asilimia 80 ya mapato ya nchi pia itatumika viwandani, katika magari na majumbani.
Akizungumza hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini alifafanua kuwa nia na madhumuni ya kujenga bomba hilo ni kukuza uchumi wa Tanzania kwani rasilimali zote asili hapa nchini ni za watanzania wote.
Katika nukuhu zake alisema “Tunajenga bomba hili kwa sababu za kiuchumi, tuna viwanda 34 vinavyotumia gesi asilia kuzalisha bidhaa, mfano kampuni moja ya kufua umeme kwa kutumia mafuta inatumia dola1.7milioni kwa siku, ndio maana tumekubalina baada ya miezi 18 tutaachana na uzalishaji wa umeme huu wa mafuta” alisema Muhongo na kuongeza;
“Umeme unaozalishwa kwa mafuta Uniti moja tunalipia Senti 30 hadi 45 ya dola za Marekani, lakini tukianza kutumia umeme wa gesi tutakuwa tukilipia Senti 6 hadi 8 ya dola.”
Hali hii imekuwa tofauti kidogo kufuatia Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema na vyama vingine pinzani kuingia katika Mkoa huo na kuwashawishi wananchi waandamane kupinga gesi hiyo kusafirishwa hadi Dar es Salaam.
Wananchi hao waliobeba mabango mengi yenye kejeli walieleza kuwa wanahitaji gesi hiyo ibaki Mtwara ili iwakomboe wananchi hao kutoka katika hali ngumu ya umaskini.
Pamoja na hayo pia Mbunge wa CCM na Mwenyekiti wa Wilaya naye pia amepinga gesi hiyo kusafirishwa.
Tovuti yako ya Habarimpya.com imeliangalia suala hili kwa upana wa hali ya juu na kugundua kuwa pengine kuna jambo ama mambo ambayo yapo nyuma ya pazia ambayo wananchi hawayabaini.
Ni kweli kuwa kukamilka kwa mradi huo kutaiondoa Tanzania kutoka katika hali ngumu ya kimaisha na kuyafanya maisha ya baadhi ya wananchi kuwa ahueni lakini ni lazima Serikali ihakikishe kuwa pande zote zinazosigana zipatane kwanza ndipo mradi huu uweze kuanza.
Tumeamua kutoa rai hii baada ya kuona kuwa hivi sasa sakata hilo pia limeingiliwa na viongozi wetu wa dini ambao nao wamesha washinikiza waumini wao kupinga vikali gesi hiyo kusafirishwa.
Sisi tunadhani kama kunauwezekano wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme mkoani humo kazi hiyo ifanyike, fedha zilizokuwa zigharamie kujenga bomba hilo la gesi sasa zigharamie kujenga mitambo ya kuzalisha umeme.
Lakini pia kama kuna uwezekano wa kuisafirisha basi elimu inatakiwa itolewe kwa wananchi wa Mtwara ili waweze kuelewa kuwa ni kwa nini gesi hiyo inasafirishwa, lakini pia mahitaji yao ya msingi kama walivyodai wanasiasa viongozi wa dini na baadhi ya watendaji wa serikali yatekelezwe.
Written by Mwandishi wetu
No comments:
Post a Comment