Thursday, January 24, 2013

Mbunge Lema hana mamlaka ya kuifunga shule

By Veronica Mheta, Arusha   
MKUU wa Wilaya ya Arusha, John Mongela
   
MKUU wa Wilaya ya Arusha, John Mongela ameamuru wanafunzi wa Shue ya Sekondari Korona iliyopo Njiro jijini hapa, warudi shuleni na kuendelea na masomo.

Amri hiyo imekuja siku chache baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kufika shuleni hapo Januari 23 mwaka huu na kuamuru shule hiyo ifungwe.

Lema aliamuru shule hiyo ifungwe kwa madai kwamba inaendeshwa kinyume na taratibu za elimu, ikiwemo kupokea wanafunzi kabla miundombinu ya shule kukamilika.

Akizungumza jana mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama na waandishi wa habari waliofika shuleni hapo, Mongela alisema Lema hana mamlaka ya kufunga shule hiyo wala kanuni za ufungaji shule za mwaka 1978 na 1995 hazimtambui mbunge mwenye kutunga sheria na kanuni kuchukua uamuzi.

Alisema kanuni zinamtambua Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi, Ofisa Elimu, walinzi wa amani au Waziri mwenye mamlaka na si Mbunge.

Alisema kama Lema alibaini shule hiyo ina upungufu, angeweza kufikisha upungufu huo kwa viongozi na kufanyia kazi na si kuibuka na utaratibu wa kuwachukua baadhi ya viongozi na kwenda nao eneo la tukio kufunga shule.

‘’Mbunge hana mamlaka ya kuifunga shule lazima viongozi tujue sheria na kanuni za kuamua tunayotaka na suala hili lisigeuzwe la kisiasa,” alisema.

Aliendelea kusema: “Hapa nikiri kuna upungufu lakini Lema anatoka eneo hili na huu upungufu anaujua, kwa nini asije tuongee na kutatua? Badala yake anaamuru shule ifungwe. Hivi hawa wanafunzi waliokosa masomo yao juzi na jana gharama yake nani atakayeilipa?

“Nasema Jumatatu ijayo wanafunzi warudi shuleni na shule haijafungwa, pia namvua madaraka Mwalimu Mkuu huyu aliyekuwepo hapa shuleni,” alisema Mongella.

Mwalimu aliyevuliwa madaraka ni John Mbise kutokana na kushindwa kusimamia shule hiyo na kukosekana kwa Bodi ya Shule. Lema alifika shuleni hapo juzi na kuamuru shule kufungwa na wanafunzi watumie ofisi yake ya ubunge iliyopo karibu na shule hiyo kujisomea na wazazi watumie pia kujadili changamoto za shule hiyo. Shule hiyo inao wanafunzi 478 lakini waliopo shuleni hapo ni 118.

Baadhi ya wanafunzi wanaishi umbali mrefu zaidi ya kilometa sita na wakati mwingine hulazimika kukodisha gari na kulipa 1,000 kila mmoja.

Wakifika shuleni hapo, hukubaliana na waalimu kupumzika kwa saa moja na inadaiwa baadhi ya wanafunzi huingia shuleni hapo saa sita na kupumzika hadi saa saba na saa nane wanarudi majumbani mwao.

Awali baadhi ya wanafunzi waliovaa kiraia ambao hawakutaka kutaja majina yao, walisema shule hiyo imeanza mwaka 2011 na wanafunzi 400 walipangwa lakini waliobaki ni 65 na kati ya hao, 30 tu ndio waliopo shuleni hapo.

No comments:

Post a Comment