Thursday, January 3, 2013

HALI YA HEWA YACHAFUKA KKKT ARUSHA,,,WAUMINI WAWAZOMEA VIONGOZI,,,,WATAKA MCHUNGAJI KIONGOZI KURUDISHWA MADARAKANI.December 30, 2012

HALI  si shwari ndani ya Kanisa la Kiinjilili la Kilutheri(KKKT) Dayosisi mkoani Arusha mara baada ya waumini wa kanisa hilo usharika wa Ngateu kuwazomea na kisha kuwafungia madhabauni baadhi ya viongozi wa kanisa hilo huku wakitishia kujitenga wakipinga kitendo cha kuvuliwa madaraka mchungaji kiongozi wa usharika huo,Phillemon Mollel.

Tukio hilo lilijitokeza tarehe 29 disemba mwaka huu majira ya saa 5;30 asubuhi ambapo baadhi ya waumini wa usharika huo walijawa na jazba na kisha kuanza kumzomea msaidizi wa askofu mkuu wa dayosisi mkoani hapa,Solomon Masangya aliyekuwa ameambatana na askofu mstaafu wa kanisa hilo,Gabriel Kimereki kanisani hapo.

Hivi karibuni kanisa hilo lilimvua madaraka mchungaji kiongozi wa usharika huo,Mollel kwa kile kinachodaiwa ni kuwashawishi waumini wa kanisa hilo wasichangie fedha za kulipa deni la hoteli inayomilikiwa na kanisa hilo ya Corridor Springs ambayo iko hatarani kupigwa mnada na benki mojawapo hapa nchini .

Hoteli hiyo inadaiwa mkopo na benki hiyo kiasi cha jumla ya $ 4 milioni sawa na sh,11 bilioni kiasi kilichopelekea kanisa hilo kuwachangisha waumini wake ili waweze kuokoa deni hilo ili isiweze kupigwa mnada wakati wowote kuanzia sasa.

Baadhi ya waumini wa usharika wa Ngateu jana walijikusanya katika viunga vya kanisa hilo katika kikao cha kupinga kuvuliwa madaraka mchungaji wao ambapo hatahivyo kikao hicho hakikufanikiwa kumalizika kwa amani.

Awali akiongea katika kikao hicho,msaidizi wa askofu wa dayosisi mkoani hapa,Masangya aliwaambia waumini hao ya kuwa amefika kanisani hapo kusikiliza kero yao na kuwataka watulize jazba kitendo ambacho kilipingwa vikali.

Hatahivyo,mara baada ya mvua kunyesha kwa wingi aliwashauri waumini hao waingia ndani ya kanisa lao ili waweze kufanya kikao hicho kwa utulivu kitendo kilichopokelewa na kisha waumini hao kuingia ndani ya kanisa hilo.

Akiwa ndani ya kanisa hilo msaidizi huyo aliibua gumzo mara baada ya kuwaambia ya kwamba anaomba akutane na baraza la wazee wa usharika huo na kisha baadaye atawapa taarifa ya kile kilichojadiliwa.

Hatahivyo,waumini hao walipinga wazo hilo kwa madai kwamba hakuna usiri wowote katika jambo hilo na kitendo cha kutaka kukutana na baraza hilo ni kutaka kuficha baadhi ya mambo ambayo wamekuwa na wasiwasi nayo.

“Jamani ndugu waumini nawaomba mtoke nje ili nikutane na baraza la wazee wa usharika wenu alafu tukimaliza kuongea nao tutawapa taarifa kamili”Masangya alisikika akiwaambia waumini

Mara baada ya vuta ni kuvute hiyo ndipo katika hali isiyo ya kawaida askofu mstaafu wa kanisa hilo mkoani Arusha,Kimerei  aliamua kuamka na kutangaza ya kwamba kikao hicho kimehairishwa hali ambayo ilichafua hali ya hewa kanisani hapo.

Hatahivyo,baadhi ya waumini waliokuwepo ndani ya kanisa hilo walianza kuwazomea viongozi hao wa kiroho na wengine wakionekana wakifunga milango ya kanisa hilo ili wasitoke nje hali iliyopelekea viongozi hao kukimbizwa katika moja ya ofisi zilizopo ndani ya kanisa hilo kwa muda lakini baadaye walitoka nje na kisha kutokomea.

Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya waumini wa kanisa hilo walisema ya kwamba endapo mchungaji wao asiporudishwa kuongoza kanisa hilo patachimbika huku wakimtaka askofu mkuu wa kanisa hilo dayosisi mkoani hapa,Thomas Laiser sanjari na katibu mkuu,Israel Ole Karyongi wote waachie ngazi.

Waumini hao walidai kwamba wako tayari kujitenga na kuanzisha dhehebu lao huku wakitangaza msimamo wa kutopeleka sadaka zao mbele ya dayosisi hiyo kwa madai kwamba kuna wamenusa harufu ya ufisadi.
“Kuanzia leo hatupeleki sadaka yoyote dayosisi na tunataka mchungaji wetu atuongoze kwenye sadaka ya mwaka mpya hatumtaki mchungaji yoyote wakitulazimisha patachiumbika hapa ni bora tujitenge”walisema kwa nyakati tofauti
Alipotafutwa Ole Karyongi hakuweza kupatikana lakini alipotafutwa Laiser alijibu kwa kifupi kwamba kwa sasa hayuko tayari kuongea chochote kwa kuwa yuko hospitalini na anapata matibabu

Chanzo cha habari na Moses Mashala.

No comments:

Post a Comment