|
Shyrose Bhanji |
NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinatarajiwa kuanza kutumia kiwango kimoja cha uzito wa magari kisichozidi tani 55.
Hiyo ni moja ya mkakati wa kuhakikisha miundombinu ya nchi hizo, hususani barabara, haziharibiwi na uzito wa magari hayo.
Pia, nchi hizo zinatarajia kuanza kutumia utaratibu mpya wa kituo kimoja cha ukaguzi, mara baada ya kukubaliana kupunguza utitiri wa vituo vya ukaguzi pale wananchi wanachama wanapoingia ndani ya nchi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 23,2013 kuhusu mafanikio ya vikao vya Bunge la Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanza kwake, Mbunge wa Bunge hilo, Shyrose Bhanji, alisema mabadiliko hayo yanatokana na miswada miwili iliyopitishwa hivi karibuni na vikao vya Bunge la EAC.
Alisema katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, Bunge hilo lilipitisha miswada miwili, ambayo ni Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Udhibiti wa Uzito wa Magari wa mwaka 2012 na Muswada wa Sheria Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kituo Kimoja cha Ukaguzi wa Mwaka 2012.
“Lengo la muswada huu wa udhibiti wa uzito wa magari ni kupunguza gharama za utengenezaji au ukarabati wa barabara za mara kwa mara na muswada huu wa umebainisha wazi kuwa kutakuwa na aina moja ya kiwango cha uzito itakayotumika kwa nchi zote za jumuiya hii,” alifafanua Bhanji, ambaye pia ni Katibu wa Wabunge wa Tanzania wa EAC.
Kuhusu muswada wa kituo kimoja cha ukaguzi, alisema umelenga kupunguza urasimu katika vituo hivyo, ambavyo kwa sasa ili mtu aweze kuingia ndani ya nchi ya jumuiya hiyo lazima akaguliwe mara mbili hivyo mara baada ya kupitishwa kwa muswada huo ukaguzi utafanyika mara moja.
“Tunataka kuondoa urasimu wa ukaguzi katika mipaka ya nchi zetu, kutakuwa na kituo kimoja tu katika kila mpaka wa nchi zetu, ambacho kitakuwa na maofisa kutoka nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Bhanji.
Alisema miswada yote miwili, iliandaliwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki.Alisema kwamba baada ya Bunge hilo kuipitisha sasa inasubiri kutiwa saini na Marais wa nchi hizo wanachama ili ianze kutumika rasmi.
Bhanji alisema tangu kuanza kwa Bunge hilo Juni mwaka jana, vikao vyake ambavyo hadi sasa ni vitano vimekuwa vikifanyika kwa awamu katika kila nchi wanachama, lakini kwa mujibu wa ratiba mpya ya Bunge hilo, mwaka ujao wa fedha, vikao vya Bunge hilo vitafanyika Arusha.
Abdullah Mwinyi ambaye ni Mbunge wa EAC, alizungumzia maendeleo ya mchakato wa soko huria na soko la forodha, ambapo alibainisha kuwa tangu kuanza kutumika kwa itifaki hizo, biashara katika nchi zote wanachama zimekua.
By Halima Mlacha