Friday, May 24, 2013

Achoma zahanati kwa wivu wa mapenzi




SEHEMU ya jengo la Zahanati ya Digarama katika Wilaya ya Mvomero, imechomwa moto na mtu anayedaiwa kufanya hivyo kutokana na wivu wa mapenzi. Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini, wanadai aliyechoma chumba kimojawapo cha zahanati hiyo, amefanya hivyo kutokana na sababu za kimapenzi.


Mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mkata aliyefanya mkutano wa hadhara na wanakijiji, baadhi yao walisimama na kudai aliyefanya kitendo hicho anadai mkewe alikuwa akifanya mapenzi na mkazi mmoja katika jengo hilo lililokuwa katika hatua za mwisho za kukamilika ili lianze kutumika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, amethibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa, mtu mmoja anahojiwa. Hakutaja jina la mtuhumiwa wala kuthibitisha kama ndiye anayetuhumiwa na wanakijiji, Kamanda Shilogile alisema atafanya hivyo uchunguzi utakapokamilika.

Imeelezwa kuwa, kama si wanakijiji kuwahi kuuzima moto ulioteketeza mbao na madirisha yote katika chumba hicho, jengo zima la zahanati hiyo lingeteketea. Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mkata, ameviamuru vyombo vya ulinzi wilayani humo kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Digarama kumsaka aliyefanya kitendo hicho.

Zahanati hiyo inatajwa kuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa Kijiji cha Digarama na vijiji jirani kutokana na kuwa mbali na Hospitali Teule ya Bwagara.

Ujenzi wa zahanati hiyo ulikuwa umekamilika kwa asilimia kubwa ikisubiriwa kufunguliwa hivi karibuni. Mkuu wa Wilaya alikutana juzi na wanakijiji na kutoa maagizo hayo.

Jengo hilo la zahanati lilichomwa usiku wa Mei 19. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya chini yake, ikiongozana na watendaji wa Idara ya Afya pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, ilifika kijijini hapo na kuitisha mkutano wa hadhara wa wananchi kulizungumzia jambo hilo.

“Moto uliotokea kwenye zahanati haukuwa wa bahati mbaya, bali ni wa makusudi uliotokana na mtu mwenye sababu zake binafsi kutaka kuteketeza kabisa Zahanati ya Kijiji cha Digarama,” alisema Mkuu wa Wilaya.

Katika mkutano huo, wananchi walielezwa faida ya zahanati na kuomba ushirikiano wa wanakijiji kubaini mhusika ili akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya , Mkata, Serikali ilitenga Sh milioni 10 kwa ajili ya ukamilishaji wa hatua za mwisho kabla ya kuifungua kuwaondolea adha ya muda mrefu waliyokuwa nayo kutokana na kukosa zahanati.

Katika mkutano huo, baadhi ya wananchi walitokwa machozi. Walidai kwa muda mrefu wamekuwa wakisafiri umbali wa zaidi ya kilometa 20 kwenda Hospitali ya Bwagara.

By John Nditi, Mvomero

No comments:

Post a Comment