Na Rashid Nchimbi wa
jeshi la PolisiArusha
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP) Liberatus Sabas akishirikiana na askari wa jeshi hilo kuharibu
mimea ya madawa ya kulevya aina ya bangi kwa kuikata kata kisha kuichoma
moto katika operesheni iliyofanyika wilayani Arumeru (Picha na Rashid
Nchimbi wa jeshi la polisi Arusha)
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP) Liberatus Sabas akibeba
begani mimea aina ya bangi tayari kwa kuikusanya kwa pamoja na kisha
kuichoma moto katika operesheni iliyofanyika wilayani Arumeru. (Picha na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP) Liberatus Sabas akichoma moto baada ya kuikusanya kwenye kundi
Askari wakipakua viroba vya madawa ya kulevya aina ya bangi toka
kwenye gari aina ya defender/Land Rover na kupakia kwenye gari kubwa
aina ya Scania mara baada ya kukusanya toka katika maeneo ya mashambani
ambapo mizigo hiyo ilifichwa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi
Arusha)
Askari wa Jeshi la polisi kutoka vikosi mbalimbali wakiwa
wanapanga mikakati kabla ya kuingia katika mashamba yaliyowazunguka
kuharibu madawa ya kulevya aina bangi na kisha kuiteketeza kwa moto
katika operesheni iliyofanyika wilayani Arumeru.
(Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Jeshila Polisi mkoani hapa kwa kushirikiana
na vyombo vingine vya Usalama limefanikiwa kuteketeza mimea aina ya bangi iliyokuwa
imeoteshwa kwenye mashamba yanayokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekari 150 kwenye vijiji
viwili tofauti vya Likamba na Imbibya ngalaoni vilivyopo wilaya ya Arumeru.
Operesheni hiyo iliyokuwa inaongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas ilianza mapema asubuhi
siku ya tarehe 01.03.2013 kwa askari hao kuingia katika mashamba mbalimbali yaliyopo
katika vijiji hivyo.
Mara baada ya kufika wilayani hapo askari hao walianza kuingia
katika kijiji cha Likamba na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na viroba
kadhaa vya bangi na kisha kuhamia kijiji jirani cha Imbibya Ngelaoni ambapo mbali
na kuendeleza operesheni ya utafutaji wa viroba vya madawa hayo lakini pia jeshi
hilo lilifanikiwa kuharibu mimea ya madawa hayo kwa kuifyeka na kisha kuiteketeza
kwa moto.
Viroba vingi vya madawa hayo vilionekana vimefichwa katika mashamba
yaliyokuwa yameoteshwa mahindi huku wenyeji wa maeneo hayo wakiyahama makazi yao
kwa muda na kukimbilia milimani.
Akizungumza katika eneo la tukio Kamanda Sabas alisema jumla ya
viroba vilivyopatikana ni 32 vyenye uzito tofauti huku watuhumiwa watatu ambao ni
JaluoTendevesi (32) na Tikayo Kilamee (23) wote wawili ni wakulima na ni wakazi
wa kijiji cha Ndevesi wilayani Arumeru pamoja na Ngwerenya Siraitei (55) Mkulima
Mkazi wa Mombo mkoa wa Tanga walikamatwa.
Kufuatia mafanikio hayo Kamanda wa Polisi mkoani hapa Kamishna
Msaidiziwa Polisi Liberatus Sabas alitoa shukrani zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha
Mh. Magesa Stanslaus Mulongo kwa ushirikiano wake mkubwa ambapo ameweza kuunganisha
vyombo vya Usalama mkoani hapa na kufanikiwa kutekeleza operesheni hiyo.
Kamanda Sabas alitumia fursa hiyo kuwaomba Wataalamu wa kilimo
kuwatembelea wakazi wa maeneo hayo kwa lengo la kuwapa elimu ya kilimo mbadala ili
ardhi hiyo waitumie kwa kulima mazao mengine ya chakula na biashara badala ya kuendelea
na kilimo cha madawa hayo haramu kwa afya ya binadamu.
Mafanikio hayo ni muendelezo wa ushirikiano mzuri baina ya jeshi
hilo na vyombo vingine vya usalama pamoja na wananchi ambao kwa kiasi kikubwa wanatoa
taarifa zinazohusu uhalifu na wahalifu kwa jeshi hilo mara kwa mara.
Kwa takriba miezi miwili, Januari na Februari 2013 jeshi hilo
limefanikiwa kukamata madawa ya kulevya aina ya Mirungi viroba 372 vikiwa vinasafirishwa
toka nchi jirani ya Kenya kuingia nchini na pia madawa ya kulevya aina ya bangi magunia yapatayo 143 huku kesi za matukio hayo
zikiwa zimeshafikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment