Monday, January 7, 2013

NYARA MBALI MBALI ZA SEREKALI ZAKAMATWA NA JESHI LA POLISI ARUSHA

by Mwandishi wa Kujitegemea

Mtuhumiwa wa nyara za serekali Peter Laurence mwenye kofia
katikati akiwa na maofisa wa jeshi la polisi chini ya ulinzi

JESHI la polisi mkoani Arusha,limekamata shehena kubwa ya nyara mbalimbali za serikali zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye ghala maalumu,eneo la Matevesi Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha,zikiwa tayari kwa kusafirishwa nje ya nchi.

Nyara hizo ni pamoja na Ngozi za Simba,Chui na Mamba ,meno ya Tembo,vichwa vya Nyani,Swala na Nyati,Pembe za kifaru,na zingine nyingi ambazo jeshi la polisi linaendelea kuzitambua.

Sambamba na hilo, jeshi hilo limemtia mbaroni mtuhumiwa wa nyara hizo aliyetambulika kwa jina la Peter Leurence (55) mkazi wa Ngaramtoni ya Chini,ambaye alikuwa akiwa amezihifadhi kwenye maboksi zaidi ya 20,kwenye nyumba yake iliyopo eneo hilo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha,Liberatus Sabas tukio la kukamatwa kwa nyara hizo limetokea jana majira ya saa 6.30 usiku wa kuamkia leo  eneo la Kisongo Mtaa wa Mateves baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Kamanda Sabas alisema kuwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa za siri majira ya saa 5 asubuhi walifika eneo la tukio majira ya saa 7 mchana na kupata upinzani mkubwa kutoka kwa walinzi wanaolinda eneo hilo kwani waliwanyima kuwapa maelekezo ya kumpata mmiliki wa nyumba hiyo.

Hata hivyo alisema kwamba askari hao waliamua kumuweka chini ya ulinzi kwa kumshurutisha mlinzi mmoja ili aweze kuwapa ushirikiano ambapo aliwapatia namba za simu na mtuhumiwa aliwaambia kuwa yupo Magugu Mkoani Manyara na angefika saa 12 majira ya jioni.

Taarifa zinadai kuwa baada ya mtuhumiwa kufika jitihada za kufanya upekuzi zilifanyika chini ya polisi wenye silaha za moto na walikuta shehena kubwa ya nyara za serekali zilizokuwa zimahifadhiwa kwenye ghala maalum na kufungwa kwenye mabox  teyari kusafirishwa kwenda kusikojulikana.

Alisema kuwa polisi waliamua kuweka ulinzi hadi kulipokucha na huku wakiendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo  na jeshi hilo linaendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo pamoja na watoto wake wawili waliokutwa wakiishi kwenye nyumba hiyo.

Aidha kamanda Sabas alisema kuwa kesho yake polisi waliendelea kufanya upekuzi na kubaini mabox zaidi ya 20 yenye nyara mbali mbali miongoni mwa nyara hizo alizitaja kuwa ni Ngozi za Chui,Simba,Tembo na Mamba pia kulikuwemo vichwa vya Nyani,Chui,Swala, Nyati,Pembe za Faru ,Meno ya Tembo na nyingine nyingi ikiwemo mfuko wa silaha inayosadikiwa kuhifadhia silaha.

 Kwa mujibu wa kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa alisema kuwa Watuhumiwa bado wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano na watafikishwa kwenye mahakama pindi upelelezi wa tukio hilo utakapo kamilika.




Ngozi ya mamba ambayo ilikutwa kwenye ghala la mtuhumiwa
ikiwa ni sehemu ya nyara mbali mbali zilizokutwa kwenye ghala hilo
ikiwemo meno ya tembo,vichwa vya simba,vichwa vya nyati,ngozi ya
simba,ngozi ya tembo na nyara nyingine nyingi za wanyama mbali
mbali.


No comments:

Post a Comment